Alhamisi tarehe 30 Januari 2020, Mhe Dkt Ramadhani Kitwana Dau, Balozi wa Tanzania nchini Malaysia ambaye pia anawakilisha Indonesia alimkabidhi Mhe Rusdi Kirana Balozi wa Indonesia nchini Malaysia Filamu za kutangaza utalii wa Tanzania . Mhe Kirana ni mfanya biashara mkubwa anaemiliki Mashirika ya ndege ya Lions Group, Batik na Malindo. Kwa pamoja, mashirika hayo yana ndege zaidi ya 300 na limeajiri wafanyakazi 43,000. Aidha mashirika hayo yanahudumia abiria 60 milioni kwa Mwaka (wastani wa abiria 160,000 kwa Siku) na ina Safari 3,400 za kwenda na kurudi kwa Siku. Mashirika hayo yanatoa Huduma za Safari kwenye zaidi ya nchi 50 duniani. Ubalozi wa Tanzania umemshawishi na amekubali kutangaza utalii wa Tanzania kwenye ndege zake kupitia inflight entertainment. Filamu hizo zitaoneshwa kwenye ndege *bila malipo* yoyote kutoka ya Serikali ya Tanzania.
Katika mazungumzo yao, Mabalozi hao wamekubaliana umuhimu wa kutangaza utalii katika ukanda wa Kusini Mashariki ya Asia ambapo Balozi Kirana ameahidi kuanzisha Safari za ndege kwenda Tanzania baada ya kufanya mazungumzo na Mawakala wa utalii wa Tanzania. Balozi huyo ameonesha utayari wake wa kukutana na kujadiliana na mawakala hao wakati wa Kongamano la Uwekezaji baina ya Tanzania na Indonesia(Tanzania/Indonesia Investment Forum) litakalofanyika Jijini Jakarta Indonesia tarehe 24-26 Septemba 2020. Aidha katika mazungumzo hayo, Mhe Dkt Dau alimwalika Mhe Balozi Kirana kutembelea Tanzania Mwaliko ambao ameukubali na ameahidi kwenda Tanzania katikati ya mwezi Septemba 2020.
